Thursday, November 29, 2012

MAKAMU MKUU WA CHUO KIKUU MZUMBE AFANYA MKUTANO NA WANACHUO!


Makamu Mkuu wa Chuo (Profesa Kuzilwa) amefanya mkutano na wanachuo wa Chuo Kikuu mzumbe "main compas". Mkutano huo ambao umehudhuliwa na wanachuo wengi kiasi cha kuutapisha ukumbi wa mikutano hali ambayo imesababisha baadhi ya wanachuo kukosa nafasi za kukaa umefanyikia katika ukumbi wa mikutano wa chuo ali maarufu NAH yaani "New Assembly Hall" kuanzia majira ya saa  8:00 mchana hadi saa 11:00 jioni.

Katika mkutano huo Makamu Mkuu wa Chuo amezungumzia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Maendeleo ya Chuo kwa ujumla katika masuala ya Taaluma, upanuzi wa miundombinu ya Chuo kama vile ujenzi wa bweni la Maria Nyerere (Mzumbe) mradi ambao umekwishakamilika na ujenzi wa Maktaba katika matawi ya Dar Es Salaam na Mbeya ambao unaendelea kwa sasa na mpango wa ujenzi wa madarasa na hostel kwa Main compas ambao upo kwenye dira ya miaka mitano kuanzia mwaka 2012-2017 baada ya dira ya mwaka 2007-2012 kukamilika kwa mafanikio makubwa.

Akiendelea na hotuba yake ambayo iliyoonekana kuvuta hisia za wanachuo ambao walikuwa na kiu kubwa na shauku ya kutaka kujua mambo mengi alielezea juu ya sheria mpya za mitihani ambazo zimeanza kutumika mwaka wa masomo 2012/2013. Ujio wa sheria hizo mpya umepokelewa kwa furaha kubwa. Suala lingine, aliloligusia ni pamoja na kucheleweshewa mikopo wanafunzi waliokuwa "Stagard semister" alisema kuwa ni sababu za kiufundi ndiyo zilizopelekea mikopo hiyo kuchelewa kwani hata yeye binafsi alikiri kufuatilia suala hilo bodi ya Mikopo.

Mambo mengine aliyoyagusia ni pamoja na kuwaasa wanachuo kutokuendesha siasa au kujihusisha  na shughuli za siasa wawapo chuoni kwani ni kinyume na sheria na 51 (1) ya Chuo Kikuu Mzumbe inayozuia uendeshaji wa shughuli za siasa ndani ya chuo. Pia amewaambia wanachuo kuwa "TCU" imetoa fursa kwa wanafunzi wanaohitaji kusoma baadhi ya mihula au kuhamia katika vyuo vingine kufuatilia maelekezo kwenye mtandao wa "TCU" kwani ni jambo linalowezekana kwa sasa. Kwa mfano, Mwanachuo anaweza kusoma muhula mmoja chuo Kikuu Mzumbe na akaenda kusoma Chuo Kikuu Dar Es Salaam Mhula unaofuata na akarudi kuendelea na masomo yake kama kawaida.

Wanachuo nao walipata fursa ya kuuliza maswali na kutoa maoni yao. Maswali mbalimbali yaliyoulizwa ni pamoja na kuwa kwanini wanachuo wanaokata rufaa ya Mitihani "appeals" wasirudishiwe karatasi za majibu, Makamu Mkuu wa Chuo, akijibu swali hilo, alisema ni jambo ambalo haliko kwenye utaratibu na kuwa haliwezekani. Swali lingine lilikuwa ni kuhusu magari ya abiria kuruhusiwa kuingia Chuoni ili kupunguza usumbufu wanaoupata wanachuo wa kutembea umbali mrefu kutoka na kwenda kituo cha magari, akijibu, Makamu Mkuu wa Chuo alisema hilo linawezekana na litafanyiwa kazi. Katika Swali la kutopewa muda wa michezo katika ratiba na ukosefu wa viwanja vya kutosha kwa ajili ya michezo nalo liliulizwa,  Makamu Mkuu wa Chuo akijibu, amesema kuwa suala la ratiba ni ufuatiliaji, nalo pia lingepatiwa ufumbuzi kwa kumshirikisha Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma (DVC A) na kuhusu viwanja, alisema lingeshughulikiwa ila aliwashauri wanachuo kufanya mazoezi mengine huku wakisubiria suala hilo kupatiwa ufumbuzi. Suala la uzembe wa walinzi limepigiwa kelele kwani kumekuwepo na wizi wa mara kwa mara na upotevu wa mali za wanafunzi kama vile Laptop na pesa taslimu nalo amesema lingefanyiwa kazi mapema.

Aidha, Mwanachuo mmoja alisikitishwa na mavazi ya wanachuo kwa sasa ambayo yanaondoa hadhi ya vitivo wanavyovisomea vya Uongozi na Sheria hasa wakina dada ambao wamefikia hatua ya kuvaa ngou zinazowaacha wazi sehemu kubwa ya miili yao hasa vifuani na kupendekeza kuwa uwekwe utaratibu maalumu wa mavazi rasmi (Dressing code) hasa muda wa vipindi ili kuweza kuleta hadhi yao na kuwatofautisha na watu wa mitaani.


Saturday, November 24, 2012

KONGAMANO LA CHANGAMOTO ZINAZOKABILI MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU NA ATHARI ZAKE LAFANYIKA CHUO KIKUU MZUMBE

Kongamano hilo la aina yake lililojumuisha wageni kutoka vyuo vikuu mbalimbali (SUA, MOROGORO UNIVERSITY, RUCO na ST. JOSEPH) waliolikwa katika kongamano hilo kubwa kuwahi kutokea vyuoni liliendeshwa na Profesa Mchome (katibu Mkuu wa TCU) kwa kushilikiana na Ndugu Onesmas Laizer (Mwakilishi kutoka Bodi ya mikopo ya Elimu ya juu) kwa kuwasilisha mada mbalimbali zilizolenga kujadili changamoto zinazoikabili bodi ya mikopo katika utoaji na urejeshwaji wa mikopo na mstakabali wa changamoto hizo. 

Mada nyingi zimejadiliwa ila mada zilizoonekana kutawala mjadala huo ni pamoja na ucheleweshwaji wa mikopo hususani chuo Kikuu Mzumbe, utoaji wa mikopo kwa upendeleo hususani wanafunzi wanaosoma kozi za sayansi jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi kupata mikopo pasipo stahili, mfano baadhi ya wanafunzi wanaofaulu masomo ya sayansi ni wale waliosoma Shule nzuri kama Fedha, St. Marian nk. kuwa wanafunzi hawa wazazi wao wanakuwa na Uwezo wa kuwasomesha, Sera ya vipaumbele "Priorities" kwa baadhi ya kozi kujenga madaraja kwani wanaokimbilia mikopo ni watoto wa masikini ambao hulazimika kusoma kozi ambazo siyo chaguo lao na malipo ya "field studies kucheleweshwa na kutolipwa kwa viwango sahihi.

Akijibu hoja hizo Ndugu Laizer amesema kuwa suala la upendeleo si kweli ni fikra tu zilizojengeka miongoni mwa watu na wanafunzi kwani mikopo hiyo hutolewa kwa kuzingatia taarifa zilizojazwa na Mwanafunzi, kuhusu ucheleweshaji ameahidi kuwa maboresho yanaendelea ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa kunakuwa na mawasiliano ya karibu na vyuo ili kuwahisha matokeo ya wanafunzi mapema  na kuwa suala hilo litabaki kuwa historia tu. kwa upande mwingine amekiri na kumesema kuwa suala hilo inawezekana lipo japo si makosa ya bodi kwani wanaamini kuwa taarifa zinazowafikia bodi zinakuwa ni sahihi kwani zinapitia kwa watenadaji wa vijiji na mitaa wanowafahamu watu. Suala la malipo ya "field studies" hutegemea na asilimia ya mkopo anaoupata mtu, hivyo kutofautiana ni jambo la kawaida.

Aidha mapendekezo yametolewa juu ya uboreshaji, mapendekezo hayo ni pamoja na uongozi wa bodi kufanya ufuatiliaji wa karibu katika taarifa zinazojazwa na wanafunzi ili kuwabaini wadanganyifu pia kufuatilia wanafunzi wanaomaliza vyuo na kuhakikisha mikopo inarudi ili kuwawezesha wanafunzi walioko vyuo kutopata matatizo ya mikopo. Mapendekezo mengine yalikuwa ni kupunguza gharama za kutuma maombi ili kuwawezesha wazazi wa kipato cha chini kumudu gharama hizo na kubadilisha mfumo unaotumika wa sasa wa kutuma maombi kwa njia ya mtandao.

Akihitimisha Kongamano hilo Profesa Itika (Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo) amewashukulu Viongozi  (kutoka TCU, HESLB na NACTE) waliohudhuria kongamano hilo na Serikali ya wanafunzi kwa ujumla.

PICHA KATIKA MATUKIO 

Ndugu Onesmas Laizer akichokoza mada katika Kongamano la Changamoto  zinazowakabili  wanafunzi wa elimu ya juu na athari zake.

Mh. Hamis Mbawala (Waziri wa Wizara ya Mikopo) Serikali ya wanafunzi Mzumbe (MUSO) akitoa maonii.


Kutoka kushoto ni Rais wa Serikali ya wanafunnzi Chuo kikuu mzumbe (MUSO), Kaimu Mkuu wa Chuo kikuu Mzumbo, Profesa Mchome (Katibu Mkuu TCU) na Katibu Mkuu wa NACTE wakifurahia jambo wakati mwakilishi kutoka bodi ya Mikopo akiwasilisha mada.



Saturday, November 17, 2012

SIKU YA MWALIMU NYERERE CHUO KIKUU MZUMBE YAFAANA, "DR. ASHA ROSE MIGILO" NDANI YA NYUMBA

Mgeni Rasmi Dr. Asha Rose Migilo akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wa Chuo pamoja na Wahadhili wa Chuo Kikuu Mzumbe.


Dr. Asha Rose Migilo akiteta jambo na Prof. F. Kamuzora Kushoto ni Pro. A. Kamuzora

Prof. Mpagala (Chuo Kikuu Dar Es Salaam) akitoa mada juu ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Afrika Mashariki.


Prof. Kopoka akiwasilisha mada ya filosofia za mwl. Nyerere na Nkwame Nkuruma juu ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Afrika Mashariki.

Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Mzumbe na "Associate Dean" wa School of Public Administration and Management (SOPAM), Rashidi Mfaume akitoa mada juu ya matatizo mbalimbali yanayovuruga Umoja na Mshikamno aliouacha Mwl. Nyerere ambayo ni ukabila na Udini unaoanza kujitokeza, mfano katika Uchaguzi wa CCM uliofanyika hivi karibuni wa kuchagua Viongozi kwa kutumia mikoa wanayotoka .

Dr. Asha Rose Migilo akifurahia jambo wakati akifuatilia moja ya mada zilizotolewa.

Viongozi wa MUSO (Waliosimama nyuma) wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi.

Siku hiyo iliyopambwa na mada mbalimbali zilizomhusisha Baba wa Taifa Hayati Mwl. Nyerere katika harakati zake za kuupigania umoja wa Afrika na ule wa Afrika Mashariki mada ambazo zilitoa changamoto kwa hali ya sasa ambayo katika hali halisi umoja huo umeanza kutoweka kutokana na vita baridi zinazojitokeza katika nchi mbalimbali za Afrika na duniani kote zinazotokea kutokana na tofauti za kidini na siasa pia na Ufukara walionao raia wa nchi hizo unaohusishwa na Viongozi wasio waaminifu (Mafisadi). 

Kwa upande mwingine imetolewa changamoto kwa vijana kutokuwa waoga katika soko la Afrika Mashariki na baadala yake kutumia fursa hiyo ili kujinufaisha kiuchumi, mfano wa fursa hizo ni pamoja na ile ya kutotozwa kodi kwa wafanyabishara wote wa bidhaa zinazozalishwa katika nchi hizo wanapokuwa wanasafirisha bidhaa zao kutoka nchi za jirani.

Akihitimisha Sherehe hiyo Mh. Prof. Daniel Mkude (Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu Mzumbe) ameomba watunga Sera za Elimu kufanya tathmini ya sera ya Elimu kuanzia shule ya Msingi ili kuwaandaa vijana kuwa na Elimu bora itakayowawezesha kupambana na changamoto mbalimbali za ajira na kuwa na umoja na hatimaye kujenga Umoja wa Nchi na Kimataifa.


Sunday, November 11, 2012

KIKAO CHA BUNGE LA SERIKALI YA WANACHUO NOVEMBA 11, 2012

Mh. Waziri Mkuu (Nasibu Kanduru) wa Serikali ya Wanafunzi Mzumbe (MUSO) akifungua  Bunge  la  kwanza  la mwaka wa  masomo  2012/2013




Wabunge wa Serikali ya wanafunzi Mzumbe (MUSO) wakifuatilia hoja mbalimbali zilizotolewa ndani ya Bunge hilo.


Mh. Naibu Spika (Christina Nelson) wa Bunge la Serikali ya wanafunzi Mzumbe (MUSO)
Katikati ni Mh. Spika (Thomas James Salala) wa Bunge la wanafunzi wa Tawi la Mzumbe , Dar  Es  Salaam  na  kulia ni Katibu Mkuu wa Serikali ya wanafunzi (MUSO)  na kushoto ni Makamu Katibu Mkuu wa Bunge la wanafunzi Mzumbe (MUSO)

Waziri wa fedha akiwasilisha hoja ya mswaada wa fedha kwa mara  ya  kwanza.

Hoja hiyo itawasilishwa tena katika Bunge hilo katika Bunge lijalo baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza na kuafikiwa na Wabunge pamoja na Serikali ijadiliwe katika Bunge lijalo ili wapate muda kuupitia muswaada huo, kuutafakari na kuuelewa na kujiridhisha ili kupitisha muswaada wanaoufahamu.
Mh. Grace Kasebele (waziri wa Katiba  na  Sheria)  akitoa  hoja  ya  kupitisha  Mswaada  wa  klabu ya Haki za Binadamu  (Human Rights Club), hoja hiyo imeungwa mkono na kupitishwa na wabunge pamoja na hoja hiyo, hoja nyingine zilizopitishwa ni pamoja na hoja za Waziri wa Elimu, Mh. Vaileth Lusana (hayupo  pichani) zilizolenga kufungua klabu mbili (Youth Career club na Pro-Poor Oriented Foundation (PPOF))

Friday, November 9, 2012

WALTER AIBUKA KIDEDEA WA EPIQ BSS 2012

Walter (Mshindi wa Epiq Bongo Star Search 2012)

Baada ya mchuano mkali wa Epiq Bongo Star Search mwaka 2012, hatimaye Mshindi wa shindano hilo apatikana na kuondoka na kitita cha pesa tasilimu za kitanzania shilingi milioni hamsini (TShs 50,000,000/=). Walter ameonekana kutoamini macho yake kiasi cha kuanguka chini na kunyanyuliwa.
Ulikuwa ni usiku mzuri kwake na mashabiki wake waliofika ukumbini kwani walionekana kumshangilia muda wote na kipindi kingine kushindwa kujizuia muda wote aliopanda jukwaani.


Thursday, November 8, 2012

MKUTANO WA WAZIRI WA ELIMU NA VIONGOZI WA MADARASA


Katika picha Baadhi ya Viongozi wakifuatilia Hotubaba ya Waziri wa Elimu 

Katika picha (Kulia ni waziri wa Elimu, Mh. Vaileth Lusana na  kushoto ni  Naibu Waziri  wa  Elimu  Mh.  Joseph  Kapyunka

Mkutano huo ulilenga kuwakaribisha viongozi wapya wa Wanafunzi na kuwaeleza kuhusu sheria mpya za mitihani, pia katika mkutano huo Viongozi wameshauliwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuyaelewa majukumu yao na kuyatekeleza kwa kufuata misingi ya kisheria.

Mh. Vaileth Lusana ambaye ni Waziri wa Elimu wa MUSO amewakumbusha Viongozi kujijengea utamaduni wa kutembelea mbao za matangazo ili kuweza kupata taarifa mbalimbali zitolewazo na Uongozi wa chuo. Aidha amewatahadharisha kutobweteka na baadala yake wasome kwa bidii ili kuwa mfano wa wanaowaongoza.

Amewataka kuwaelimisha wanafunzi wenzao juu ya sheria za Mitihani na kuzizingatia wawapo kwenye vyumba vya mitihani kwani kufanya hivyo kutawaepusha na matatizo yasiyo ya lazima. 

Wednesday, November 7, 2012

OBAMA ACHAGULIWA TENA KUIONGOZA MAREKANI

Rais Baraka Obama amechaguliwa tena kuiongoza Marekani kwa mara nyingine. Ushindi huo umepelekea majonzi kwa wanachama wa Republican kwa kutoamini kilichotokea dakika 60 za mwisho zilizompa ushindi rais Baraka Obama. Hata hivyo mpinzani wake Mitt Ronney amempongeza Baraka Obama kwa ushindi huo na kukubali kuwa amemshinda na hana budi kufanya hivyo kwani ndiyo chaguo la wamarekani. 

Kwa upande mwingine, ilikuwa ni furaha kubwa kwa wanachama wa Democrats kwa ushindi walioupata. Amewashukulu kwa kumchagua na kurudi Ikulu kwa mara nyingine, aidha amesema kuwa ushindi huo ni wa wamarekani wote bila kujali chama na majimbo wala waliomchagua au la na kusema kuwa kila mtu ana maoni yake binafsi na wamefanya maamuzi sahihi. Amewataka kutokusahau sera ya Marekani kuwa ni umoja, kazi na uzalendo ambayo imewafanya kuwa na mafanikio makubwa kuliko nchi yoyote duniani. 

UONGOZI WA MUSO UNAMPONGEZA RAIS BARAKA OBAMA KWA KUCHAGULIWA TENA KUIONGOZA NCHI YA MAREKANI. TUNAMTAKIA MAFANIKIO MEMA KATIKA KIPINDI CHOTE CHA UONGOZI WAKE.

UCHAGUZI WA VIONGOZI WA MABWENI (HOSTEL REPRESENTATIVES) KUFANFYIKA JUMAMOSI TAREHE 10/11/2012

Mh. Elly Masoka, (Naibu waziri wa Katiba na Sheria Serikali ya Wanachuo Chuo Kikuu Mzumbe (MUSO)) anawatangazia wanachuo wote wa Mzumbe ya kuwa kutakuwa na Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika jumamosi kuanzia saa 4:00 Asubuhi. 

Wanachuo wote wa Mabweni husika wenye nia ya kugombea nafasi hizo wanakumbushwa kutumia nafasi hiyo kikatiba kwa kujiandikisha majina yao kwa Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Mh. Elly Masoka kupitia Namba ya simu 0719 771115 au 0765 097537

Saturday, November 3, 2012

BARAZA LA WANACHUO CHUO KIKUU MZUMBE LAFANYIKA

Mh. Amon Chakushemeire Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa  Chuo Kikuu  cha  Mzumbe  (MUSO)  akisoma hotuba  yake   kwenye Baraza la Wanachuo wa Chuo Kikuu Mzumbe, hotuba hiyo imewavutia wanachuo kwani imegusa matarajio yao kwa kiasi kikubwa na walionekana kufuatilia kwa makini na pia ilipongezwa na wanachuo hao ambao walipata nafasi ya kutoa maoni na kuuliza maswali. Kati ya mambo yaliyokonga mioyo ya wanachuo ni pamoja na suala la mabadiliko ya sheria za mitihani, Mikopo ya wanachuo kutoka bodi ya Mikopo hasa kwa kuwa walikuwa na shauku ya kujua hatima ya wanafunzi waliositishiwa mikopo yao kwa kupata "Supplementary", ambapo aliwahakikishia kuwa lilikuwa limeshashughulikiwa na wangeendelea kupata mikopo yao baada ya taratibu zote kukamilika, Aidha amewataka wanafunzi kuelewa mipaka ya Viongozi wao katika kufuatilia baadhi ya mambo na kuwaondoa wasiwasi wanachuo kwa kuwaomba wapuuze baadhi ya fikira potofu kutoka kwa watu wanaotaka umarufu wa kisiasa kwa madai kuwa Serikali haiwajali na kuwa haifuatilii matatizo yao na baadala yake kujenga utamaduni wa kufuatilia mambo muhimu kwa kupata taarifa kutoka sehemu husika (Viongozi wao) na si maneno yanayosemwa na wanafunzi wenzao. Akiongea kwa masikitiko makubwa alitoa mfano wa baadhi ya Habari ambayo ilikuwa ni ya uzushi na ambayo iliusikitisha Uongozi wa Chuo ya kuwa Chuo kilikuwa kikiweka pesa kwenye "fixed Account" zinazotoka Bodi ya Mikopo na kuwacheleweshea wanafunzi kwa makusudi, jambo ambalo halikuwa sahihi.

Wanachuo wakifuatilia kwa makini hotuba ya Rais wa Serikali ya Wanafunzi  Mzumbe (MUSO) katika Baraza la wanachuo  lililofanyika katika ukumbi wa National Assembly Hall maarufu kama NAH, Baraza hilo lilivunja rekodi ya mahudhurio ya miaka yote kwa kuhudhuliwa na wanachuo wengi. Wanachuo walionekana kuvutiwa na hotuba hiyo iliyovuta hisia zao, hasa pale alipogusia mambo mbalimbali ambayo serikali imefanikiwa kuyafanya kwa kipindi cha uongozi wake ikiwa ni kupata Sheria mpya za mitihani (Examination by-laws), Sheria ambazo zimekuwa ni   kiu kubwa ya wanafunzi wa Chuo kikuu cha Mzumbe, utatuzi wa tatizo la nyenzo za kufundishia (Audio systems na VLCDs) katika madarasa mbalimbali na upanuzi wa mawasiliano ya Internet (Wireless Extension) ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wa mtandao. 

RAIS WA SERIKALI YA WANAFUNZI MZUMBE (MUSO) AFANYA UTEUZI WA MAWAZIRI NA MANAIBU WAZIRI

Mh. Amon Chakushemeire, Rais wa Serikali ya Wanafunzi Mzumbe (MUSO) amefanya uteuzi wa Mawaziri na Manaibu Waziri wa Wizara mbalimbali na kuwahamisha Wizara baadhi ya Manaibu Waziri. Katika uteuzi huo baadhi ya Manaibu Waziri wamepandishwa hadhi na kuwa Mawaziri kamili wa Wizara. Manaibu Waziri waliopandishwa hadhi ya kuwa Mawaziri ni pamoja na Mh. Judith Kweka aliyekuwa N/Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge na kuwa Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mh. Hamis Mbawala aliyekuwa N/Waziri wa Wizara ya Mikopo, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Wizara ya Mikopo, Mh. Vaileth Lusana Naibu Waziri Wizara ya Elimu, Teknolojia na Mafunzo ya Sanaa, amekuwa Waziri kamili wa Wizara hiyo, Mh. Mfaume Mfaume aliyekuwa Naibu Waziri Wizara ya Afya, Chakula na Mahusiano amekuwa Waziri katika Wizara hiyo, Mh. Albert Nzilolela Naibu Waziri  Wizara ya Habari na Mawasiliano  kwa sasa ni Waziri wa Wizara ya Habari na Mawasiliano na Mh. Lydia Yohana aliyekuwa Naibu Waziri Wizara ya Mazingira, Maji na Nishati amekuwa Waziri wa Wizara husika.

Aidha Mh. Rais amefanya mabadiliko katika Wizara mbalimbali kwa kufanya uteuzi wa Mawaziri, Manaibu Waziri na Katibu wa Kudumu wa Wizara, Mawaziri waliobahatika kuteuliwa katika nafasi hizo ni Mh. Grace Kasebele Waziri wa Wizara ya Sheria na Katiba, Mh. John Lameck Waziri Wizara ya Malazi na Miundombinu, Joseph Kapyunka Naibu Waziri Wizara ya Elimu, Teknolojia na Mafunzo ya Sanaa, Mh. Robert Tende Naibu Waziri wizara ya Vijana, Utamaduni na Michezo na Mh. Gigwa Mipawa Katibu wa Kudumu Wizara ya Elimu, Teknolojia na Mafunzo ya Sanaa.

Ili kuleta ufanisi na tija katika utendaji kazi, Mh. Rais wa Serikali ya Wanafunzi Mzumbe (MUSO) amefanya mabadiliko mbalimbali kwa kuwahamisha Wizara baadhi ya Manaibu Waziri wa wizara mbalimbali. Manaibu waliohamishwa Wizara ni pamoja na Mh. Ebenezer F. Elishiwanga kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na kuhamishiwa Wizara ya Sera, Uratibu na Shughuli za Bunge na Mh. Hellen Said aliyekuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Fedha, Mipango na Uwekezaji amekuwa Naibu Waziri Wizara ya Sera, Uratibu na Shughuli za Bunge.

Zaidi, Mh. Rais wa Serikali ya Wanafunzi Mzumbe (MUSO) amewaapisha Wateule hao na kuanza kazi mara moja katika nafasi walizoteuliwa mara baada ya kula kiapo hicho. Mara baada ya kuwaapisha, Mh. Rais amewakumbusha kuwa na moyo wa kuwatumikia Wanachuo na kuwaasa kutii kiapo hicho kwa kuzingatia maneno yaliyomo na maadili ya Uongozi.
 
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

IDADI YA WASOMAJI

RedEnvelope
. .

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...