Social Icons

USRC meeting

Saturday, January 26, 2013

RAIS WA SERIKALI YA WANACHUO MZUMBE AAPISHWA



Na Albert Nzilolela

Rais mteule, Mh. Lukiko Lukiko wa Serikali ya wanafunzi Mzumbe (MUSO) ameapishwa katika ukumbi wa NAH na kufuatiwa na hafla ya kumpongeza iliyofanyika katika hotel ya Lumumba Complex Mzumbe. Kabla ya kuapishwa, alitanguliwa na hotuba ya Rais anayemaliza kipindi chake cha uongozi na Mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi. Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro aliyewakilishwa na Afisa Utumishi wa Mkoa Ndugu Elias Andrew.

Rais anayemaliza muda wake Mh. Amon Chakushemeire amewashukulu sana wanachuo kwa kumuamini na kumchagua kuiongoza Serikali ya wanachuo (MUSO). Katika hotuba yake ameushukulu uongozi wa Chuo pamoja na Baraza la mawaziri na Bunge la wanachuo kwa kumpa ushirikiano wa hali juu kwani anaamini kuwa ushirikiano huo ndiyo umepelekea yeye kumaliza muda wake kwa heshima kubwa na mafanikio makubwa. Pia alionesha kusikitishwa na dhana ya wanachuo kudhani kuwa wana ufahamu wa kila jambo kwa kutojali kusoma hata matangazo yanayowahusu suala linalopelekea kutokuhudhuria semina na midahalo mbalimbali inayofanyika chuoni. Lakini pia amekiri kuwa ni kazi ngumu sana kuwaongoza wasomi.

Mwenyekiti wa tume amezungumzia changamoto mbalimbali zinazoikumba tume ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na bajeti finyu kwa ajili ya kuendeshea shughuli za uchaguzi, upatikanaji wa taarifa za wanafunzi kwa muda, wanafunzi  kutokuwa na hulka ya kusoma matangazo suala ambalo lilipelekea wagombea wengi kurejesha fomu za kuteuliwa kuwa wagombea kwa kuchelewa, upatikanaji wa mwenyekiti wa tume kwa kigezo cha kuwa mtu mwenye uelewa au taaluma katika masuala ya sheria kuwa kinawanyima haki wanachuo wengine kugombea nafasi hiyo.

Baada ya hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Rais mteule na makamu wake Mh. Teddy Ladislaus wameapishwa na kufuatiwa na hotuba ya Rais huyo, Mh. Lukiko Lukiko. Katika hotuba yake amewashukulu wanachuo kwa kumpa nafasi hiyo kubwa ya kuiongoza serikali ya MUSO. Aidha, Rais Lukiko amesema kuwa anaamini kuwa njia sahihi ya kufanikisha jambo lolote ni kwa njia ya majadiliano na ushirikiano.

Aidha Rais Lukiko amewahakikishia wanachuo waliofika katika hafla hiyo ya kuapishwa kwake kuwa angejitahidi kuweka mazingira bora ya kuwafanya wanachuo wapate mafanikio mazuri kitaaluma. Amegusia mambo mbalimbali ya kijamii kama vile unyanyapaaji wa waathirika wa UKIMWI, Rushwa, Chuki zinazotokana tofauti za kisiasa pamoja na mifumko ya bei za vitu. Ameahidi kuandaa midahalo mbalimbali ya majadiliano ili kutoa elimu juu ya changamoto hizo ambazo ni vikwazo vya maendeleo pia ametoa wito kwa wasomi kutumia elimu yao kusaidia jamii zinazowazunguka hasa watu wa vijijini.
Hotuba ya Rais Lukiko imefuatiwa na hotuba ya Profesa Kamuzora (Kaimu Makamu mkuu wa Chuo) ameipongeza serikali iliyomaliza muda wake kwa umahili mkubwa na ufanisi katika utendaji kazi wake na kumaliza muda wake pasipokuwa na matatizo yoyote na kukili kuwa hakuamini kuwa muda wa uongozi ulikuwa umeisha kwani aliona kuwa ni muda mfupi sana kwa kusema kuwa ameona kama siku zilikuwa zimekimbia sana kwa upande mwingine amempongeza Rais aliyekuwa anamalizia muda wake Mh. Amoni Chakushemeire kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TAHLISO na kusema kuwa hiyo inadhihirisha kuwa ni Kiongozi bora na mtu anayekubalika si ndani ya chuo bali hata nje ya mipaka ya chuo pia amempongeza Rais mpya Mh. Lukiko Lukiko kwa kuaminiwa na kuchaguliwa na wanachuo na kusema kuwa amechaguliwa kuwaongoza wanachuo hivyo hana budi kuwatumikia kwa bidii. Amewashauri wanafunzi kujenga tabia ya kutumia “website” ya chuo na “blog” ya MUSO kupata taarifa mbalimbali zinazohusiana na chuo kwani suala la matumizi ya mbao kwa ajili ya matangazo litasitishwa mara moja hivi karibuni.

Baada ya hafla hiyo ya kuapishwa lilifuatia tukio ya sherehe ya kumpongeza iliyofanyikia katika hoteli ya Lumumba Complex iliyoko Mzumbe. Katika sherehe hiyo wazazi walipata fursa ya kumpongeza Rais Lukiko. Baba mzazi, Ndugu Ilvin Mgeta amempongeza mwanae na keahidi kuwa atampa ushirikiano katika kipindi chake cha Uongozi, pamoja na pongezi hizo amemtahadharisha Rais Lukiko kuwa kazi aliyopewa ni kubwa na ina majukumu makubwa hivyo amemtaka kutumia muda wake vizuri ili kuhakikisha haporomoki kimasomo.

MATUKIO KATIKA PICHA


Mh. LUKIKO LUKIKO (RAIS MTEULE WA SERIKALI YA WANAFUNZI)  AKIAPISHWA

Mh. TEDDY LADISLAUS (Makamu wa Rais wa Serikali ya wanachuo MUSO)  AKIAPISHWA

Mh. Lukiko Lukio Rais Mteule (kulia) akiwa na Mh. Amon Chakushemeire (kushoto) Rais anayemaliza muhula wake
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Ndugu Mwashibanda Shibanda akitoa tathmini ya Uchaguzi wa mwaka 2013

Mama mzazi wa Rais Lukiko, Mrs. Yusta Mgeta akimpongeza mwanae kwa kuchaguliwa 

Baba mzazi wa Rais Lukiko, Ndugu Ilvin Mgeta akimpongeza mwanae katika sherehe ya kumpongeza Rais iliyofanyika Lumumba complex. 

Baadhi ya Viongozi wa MUSO (mbele) na wanachuo wakishuhudia Rais wa Serikali ya MUSO pindi akiapishwa

Viongozi wa MUSO wakifuatilia kwa makini matukio mbalimbali ya kuapishwa kwa Rais Lukiko.


Sunday, January 13, 2013

HATIMAYE RAIS WA MUSO APATIKANA


Na Albert Nzilolela

Baada ya mbwembwe nyingi za kampeni za Urais wa Serikali ya Wanafunzi Mzumbe (MUSO) zilizodumu kwa muda wa siku nane mfululizo hatimaye Rais mteule wa MUSO apatikana. Wagombea wa Urais waliokuwa kwenye kinyang'anyiro hicho cha kugombea nafasi hiyo kubwa ya Serikali ya wanafunzi ni pamoja na Lukiko Lukiko (Faculty of Law), Nicas Mahinda (School of Business) na Nicolas Magere (Faculty of Social Science).

Matokeo ya kula zilizopigwa yalikuwa kama ifuatavyo; Lukiko Lukiko ameongoza kwa kupata kula 977 akifuatiwa na Nicolas Magere aliyepata kula 850 nafasi ya tatu ilichukuliwa na Nicas Mahinda aliyejinyakulia kula 579. kwa matokeo hayo Mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi, Ndugu Mwashibanda Shibanda alimtangaza Lukiko Lukiko kuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi Mzumbe (MUSO) na Makamu wake atakuwa ni Bi Teddy Ladislaus kutoka Faculty of Science and Technology ambaye alikuwa ni mgombea mwenza katika kinyang'anyiro hicho cha kugombea. Wagombea wenza wengine waliofanikiwa kugombea nafasi hiyo ni pamoja na Jackline Daniel (School of Public Administration and Management) aliyekuwa mgombea mwenza wa Ndugu Magere na Frida Methusela (School of Public Administration and Management) mgombea mwenza wa Nicas Mahinda ambaye alikuwa amepewa nafasi kubwa ya kushinda nafasi hiyo lakini akaambulia nafasi ya mwisho.

Rais mteule anatarajiwa kuapishwa tarehe 25/01/2012 ambapo mara baada ya kiapo hicho ataanza rasmi majukumu ya kuitumikia Serikali ya Wanafunzi (MUSO).

Tuesday, December 25, 2012

MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI WA VIONGOZI MUSO AWATANGAZIA WAGOMBEA KUCHUKUA FOMU


Na Albert Nzilolela

Mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi MUSO, Ndugu Mwashibanda Lukas Shibanda amewatangazia Wagombea mbalimbali wenye nia ya kugombea nafasi za Uongozi wa Serikali ya Wanafunzi Mzumbe (MUSO) kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo kuanzia tarehe 26/12/2012 hadi tarehe 28/12/2012. Muda wa kuchukua fomu utakuwa ni kuanzia saa 4:00 Aasubuhi hadi saa 10:00 jioni. Na kuwa mwisho wa kurejesha fomu hizo ni tarehe 29/12/2012. Nafasi zilizotangazwa kugombewa ni pamoja na Rais, Makamu wa Rais, Seneta, School Representatives (SRs) na Faculty Representatives (FRs).

Aidha, Mwenyekiti huyo ametoa tahadhari kwa wale wanaoanza kupiga kampeni ya kuwa muda wa kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria bado haujatangazwa na tume, na kuwa kuyafanya hivyo ni kinyume na sheria ya Uchaguzi kifungu cha sheria Na. 46 (2). Na kusema kuwa Mgombea yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa nafasi ya Ugombea katika nafasi husika.

Saturday, December 22, 2012

TUME YA UCHAGUZI WA VIONGOZI WA SERIKALI YA WANAFUNZI MZUMBE YAUNDWA

Na Albert Nzilolela (Waziri wa Habari na Mawasiliano)

Kikao cha Bunge la Serikali ya Wanafunzi (MUSO) kimefanyika na kumalizika kwa kuchagua tume huru ya Uchaguzi ambayo inaundwa na wajumbe kumi ambao walimchagua Mwenyekiti wa Kamati hiyo, makamu mwenyekiti na Katibu wa Kamati hiyo.

Bunge hilo ambalo lilikuwa ni la Mwisho limeahilishwa kwa kuvunjwa na Mh. Rais wa Serilkali ya Wanachuo (MUSO).

Bunge limeanza kwa utangulizi wa hotuba ya Mh. Frenk Mbialu (Spika wa Bunge la Serikali ya Wanachuo - MUSO), ameanza kwa kuwashukulu wabunge kwa kuonesha Ushirikiano kwa kipindi chote chake cha Uongozi kilichomalizika baada ya Rais kulihotubia na kulivunja Bunge hilo. Katika hotuba hiyo ya utangulizi aliwasihi sana Wabunge kupitisha Sheria ya Matumizi ya fedha ili kuleta dhana ya uwajibikaji kwa serikali itakayokuwa madarakani kwa Mwaka wa masomo 2013 na ndpo alipomkaribisha Waziri Mkuu kufungua kikao hicho rasmi.

Waziri Mkuu ameanza kwa kutoa taarifa ya Uchaguzi wa Jumuiya ya Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO ) ambao Rais wa MUSO aliibuka Mshindi na kuwa Mwenyekiti wa TAHLISO, hivyo amempongeza Rais kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TAHLISO. Pia alichukua nafasi hiyo kuwashukulu Wabunge kwa Ushirikiano waliouonesha kwa kipindi chote Serikali ilipokuwa madarakani.

Miswada mbalimbali imejadiliwa katika Bunge hilo, miswaada iliyotawala katika Bunge hilo ilikuwa ni pamoja na ule wa Sheria ya matumizi ya fedha, mapendekezo ya mchango  wa TShs 5000/= itakayokuwa inakatwa kwenye pesa ya "Caution money" ambao unalenga kuchangia ujenzi wa mabweni, kusaidia wanafunzi wenye matatizo na gharama za masomo kwa Wanachuo wanaosoma nje ya nchi katika prrogramu ya kubadilishana (Exchange programs), michango ilipendekezwa na jumuiya ya wanachuo waliohitimu Mzumbe (Mzumbe University Convocation). Mswaada mwingine ni pamoja na ule wa Mchango wa Bima ya kifo (Funeral Assurance) TShs. 2500/= kuchangiwa na wanachuo, pendekezo lililoletwa kwa Serikali ya wanachuo na Kampuni ya AFRICAN LIFE ASSURANCE ambayo makao yake makuu ni Afrika ya Kusini ambapo mwanachama anayefariki familia yake hufaidika kwa kupewa TShs. 800,000/=.

Miswaada yote imejadiliwa na Mswaada wa Sheria ya Matumizi ya fedha umepitishwa kwa mapendekezo kuwa sheria hiyo ifanyiwe marekebisho baadhi ya vipengele vyenye mapungufu. Mswaada wa Michango ya Funeral Assurance na ule wa michango uliopendekezwa na jumuiya ya Wanachuo wa Mzumbe waliohitimu miaka ya nyuma haikuweza kupitishwa. Wabunge walipendekeza kuwa Miswaada hiyo ijadiliwe kwenye Baraza la wanachuo na kuletwa Bungeni katika Bunge linalofuatia ili ijadiliwe.

Wabunge wamefanikiwa kuchagua Kamati ya Uchaguzi itakayoratibu Uchaguzi wa Viongozi wa MUSO (FRs, SRs, Senators na Rais), Tume hiyo inayoundwa na ajumbe kumi (10) ilifanikiwa kumpata Mwenyekiti, Mwenyekiti Msaidizi pamoja na Katibu wa kamati hiyo. Aliyefanikiwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti ni Mh. Mashibanda, Mwenyekiti Msaidizi ni Ester Charles na nafasi ya katibu imechukuliwa na Paul Samwel.

Mh. Rais wa Serikali ya Wanachuo, Amon Chakushemeire ameahilisha na kuvunja Bunge kwa kuainisha mafanikio ambayo Serikali imeyatekeleza kwa kipindi chake cha Uongozi ikiwa ni pamoja na Matokeo ya wanachuo kutolewa kwenye ARIS, kuiunganisha MUSO na jumuiya ya Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (EAUSC) na TAHLISO, kuunganisha DSTV ambapo wanachuo huangalia mpira bure, Mifumo ya sauti (Audio systems)vyumba vya mihadhara, kuimalishwa kwa mfumo wa Intanet, Makongamano ya kitaaluma, kupunguza gharama ya mawasiliano kwa kushilikiana na mitandao mbalimbali mfano Airtel (mfumo wa Boom) ambao umepunguza gharama za mawasiliano kwa kiwango kikubwa, kuwagharimikia gharama za chakula (mill accomodation) wanafunzi wanne kutekeleza sera ya Serikali ya kuwapa nafasi wanawake ambapo Serikali yake iliindwa na asilimia 55% ya Wanawake, NMB ATM na kubwa zaidi kufanikiwa kupata Sheria mpya za mitihani. 

Mwisho Rais amewaponongeza wajumbe waliochaguliwa katika tume ya Uchaguzi na kuwashukulu wabunge kwa kutoa Ushirikiano mzuri kwa kipindi chake cha Uongozi ambacho kilikuwa kinaelekea kumalizika ndani ya mwezi mmoja baada ya Rais kuapishwa. amemaliza kwa kutoa angalizo na ushauri kwa baadhi ya wabunge kujitambua kuwa wao ni sehemu ya Serikali na hivyo kutokuonesha hali ya Usariti katika Serikali ijayo.

Bunge limevunjwa rasmi na Mh. Rais wa MUSO na kabla ya kuvunja bunge hilo alitanguliwa na hotuba  ya Mh. Frenk Mbialu (Spika wa Bunge la Serikali ya Wanafchuo Mzumbe (MUSO). Katika hotuba yake ya mwisho kwa Bunge amempongeza Rais kwa kuiongoza Serikali kwa mafanikio makubwa hasa kwa kufanikiwa kutunga sheria ya Matumizi ya fedha iliyopitishwa kwa kishindo, kufanikisha kupatikana kwa sheria mpya za mitihani kutekeleza baadhi ya ahadi alizoahidi katika ilani yake.


PICCHA KATIKA MATUKIO



Mh. Chakushemeire, Rais wa Serikali ya wanafunzi MUSO akisoma hotuba yake Bungeni, hotuba iliyofuatiwa na kuvunjwa kwa Bunge la Serikali ya Wanafunzi la mwaka 2012.

Mh. Frenk Mbialu, Spika wa Bunge la Serikali ya wanafunzi MUSO akifungua kikao cha Bunge.

Mh. Kamihanda (Mbunge) akichangia hoja ya Mswaada wa Sheria ya matumizi ya Fedha.

Wabunge wakila kiapo cha utii cha kuitumikia Serikali ya Wanafunzi (MUSO).

Wajumbe wa tume huru ya Uchaguzi wa Serikali ya wanafunzi wakisubili kiapo cha utii, kutoka kulia ni Viongozi wa tume hiyo Ndugu Paulo Samwel (Katibu), Ndugu Ester Charles (Mwenyekiti Msaidizi) na Ndugu Mashibanda Lukas (Mwenyekiti).

Waheshimiwa Mawaziri wa Serkali ya Wanafunzi (MUSO) wakifuatilia kwa makini hotuba ya Rais .

Mh. Justus, Waziri wa fedha akiwasilisha Bungeni Mswaada wa sheria ya matumizi ya fedha. 

Mh. Kanduru, Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi (MUSO) akifungua kikao cha Bunge.

Wabunge wapya wakila kiapo cha kuitumikia Serikali ya Wanafunzi (MUSO).
Watambue Viongozi wa Tume huru Ya Uchaguzi (MUSO)

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi MUSO, Ndugu Mwashibanda Lukas Shibanda
Makamu Mwenyekiti Uchaguzi MUSO, Ndugu Ester Charles
Katibu wa Tume ya Uchaguzi MUSO, Ndugu Paul Samwel




Saturday, December 1, 2012

CHUO KIKUU MZUMBE WASHINDI WA MPIRA WA KIKAPU!


Mzumbe imeibuka mshindi wa mashindano ya mpira wa kikapu katika mashindano ya mpira huo yaliyofanyika St. Jordan University college iliyopo nje kidogo ya Mji wa Morogoro. Mashindano hayo yamejumuisha Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Mzumbe na St. Jordan yalikuwa mashindano makali kiasi cha kutoana jasho lakini hata hivyo kwa kuwa mshindi siku zote lazima apatikane, Mzumbe waliibuka kidedea mbele ya SUA na kubeba kombe hilo. 

Mashindano hayo yaliyoandaliwa kwa hisani ya Benk ya CRDB yamejumuisha pia mchezo wa mpira wa Miguu na Pete ambapo Mzumbe waliibuka washindi wa pili na kupata kikombe cha mshindi wa pili kwenye mchezo wa mpira wa miguu pamoja na medali za shaba baada ya kushindwa kwa magoli mawlili kwa Nunge (Mzumbe 0, St. Jordan 2) katika mchezo wa fainali, pia katika mpira wa pete Mzumbe imejinyakulia medali za shaba kwa kuwa mshindi wa pili nyua ya St. Jordan netball Team ambayo imeshika nafasi ya kwanza kwa pointi 45 ambapo Mzumbe Netball Team imepata point 40 na kufuatiwa na SUA netball Team iliyopata jumla pointi 20.

Katika mashindano hayo Mzumbe imefanikiwa kumpata mchezaji bora wa Kikapu Mzee wa kudanki (Emmanuel) na kuzawadiwa medani ya dhahabu. Aidha kulikuwa na mkali wa kucheza na maiki, mtangazaji bora mwenye kipaji cha pekee kutoka Mzumbe ambaye ameongoza matangazo ya mpira wa miguu kwa kushirikiana na vyombo vya habari, Mbaraka Tombo ambaye ameibuka na medani ya Shaba kwa kuwa mtangazaji bora wa vyuo vyote vitatu.

PICHA KATIKA MATUKIO

Marefarii wasaidizi mpira wa pete wakiwa kazini

Timu ya mpira wa pete St. Jordan University college wakiwa kwenye pozi

Timu ya mpira wa pete ya SUA iliyoshiriki mashindano.

Timu ya Mpira wa pete ya Mzumbe ikiwa kwenye picha na Naibu  Waziri wa Michezo Mzumbe, Mh. Robert Tende (Kushoto) na Kulia ni Ndugu Maganga, Refarii wa mchezo huo wa Pete kutoka St. Jordan 

Timu ya mpira wa Miguu ya Mzumbe ikiwa kwenye pozi pamoja na Waziri wa Michezo (kulia) Mh. Dennis Kato

Timu ya mpira wa volleyball ikiwa kazini (Kushoto ni Timu ya Mzumbe)


Thursday, November 29, 2012

MAKAMU MKUU WA CHUO KIKUU MZUMBE AFANYA MKUTANO NA WANACHUO!


Makamu Mkuu wa Chuo (Profesa Kuzilwa) amefanya mkutano na wanachuo wa Chuo Kikuu mzumbe "main compas". Mkutano huo ambao umehudhuliwa na wanachuo wengi kiasi cha kuutapisha ukumbi wa mikutano hali ambayo imesababisha baadhi ya wanachuo kukosa nafasi za kukaa umefanyikia katika ukumbi wa mikutano wa chuo ali maarufu NAH yaani "New Assembly Hall" kuanzia majira ya saa  8:00 mchana hadi saa 11:00 jioni.

Katika mkutano huo Makamu Mkuu wa Chuo amezungumzia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Maendeleo ya Chuo kwa ujumla katika masuala ya Taaluma, upanuzi wa miundombinu ya Chuo kama vile ujenzi wa bweni la Maria Nyerere (Mzumbe) mradi ambao umekwishakamilika na ujenzi wa Maktaba katika matawi ya Dar Es Salaam na Mbeya ambao unaendelea kwa sasa na mpango wa ujenzi wa madarasa na hostel kwa Main compas ambao upo kwenye dira ya miaka mitano kuanzia mwaka 2012-2017 baada ya dira ya mwaka 2007-2012 kukamilika kwa mafanikio makubwa.

Akiendelea na hotuba yake ambayo iliyoonekana kuvuta hisia za wanachuo ambao walikuwa na kiu kubwa na shauku ya kutaka kujua mambo mengi alielezea juu ya sheria mpya za mitihani ambazo zimeanza kutumika mwaka wa masomo 2012/2013. Ujio wa sheria hizo mpya umepokelewa kwa furaha kubwa. Suala lingine, aliloligusia ni pamoja na kucheleweshewa mikopo wanafunzi waliokuwa "Stagard semister" alisema kuwa ni sababu za kiufundi ndiyo zilizopelekea mikopo hiyo kuchelewa kwani hata yeye binafsi alikiri kufuatilia suala hilo bodi ya Mikopo.

Mambo mengine aliyoyagusia ni pamoja na kuwaasa wanachuo kutokuendesha siasa au kujihusisha  na shughuli za siasa wawapo chuoni kwani ni kinyume na sheria na 51 (1) ya Chuo Kikuu Mzumbe inayozuia uendeshaji wa shughuli za siasa ndani ya chuo. Pia amewaambia wanachuo kuwa "TCU" imetoa fursa kwa wanafunzi wanaohitaji kusoma baadhi ya mihula au kuhamia katika vyuo vingine kufuatilia maelekezo kwenye mtandao wa "TCU" kwani ni jambo linalowezekana kwa sasa. Kwa mfano, Mwanachuo anaweza kusoma muhula mmoja chuo Kikuu Mzumbe na akaenda kusoma Chuo Kikuu Dar Es Salaam Mhula unaofuata na akarudi kuendelea na masomo yake kama kawaida.

Wanachuo nao walipata fursa ya kuuliza maswali na kutoa maoni yao. Maswali mbalimbali yaliyoulizwa ni pamoja na kuwa kwanini wanachuo wanaokata rufaa ya Mitihani "appeals" wasirudishiwe karatasi za majibu, Makamu Mkuu wa Chuo, akijibu swali hilo, alisema ni jambo ambalo haliko kwenye utaratibu na kuwa haliwezekani. Swali lingine lilikuwa ni kuhusu magari ya abiria kuruhusiwa kuingia Chuoni ili kupunguza usumbufu wanaoupata wanachuo wa kutembea umbali mrefu kutoka na kwenda kituo cha magari, akijibu, Makamu Mkuu wa Chuo alisema hilo linawezekana na litafanyiwa kazi. Katika Swali la kutopewa muda wa michezo katika ratiba na ukosefu wa viwanja vya kutosha kwa ajili ya michezo nalo liliulizwa,  Makamu Mkuu wa Chuo akijibu, amesema kuwa suala la ratiba ni ufuatiliaji, nalo pia lingepatiwa ufumbuzi kwa kumshirikisha Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma (DVC A) na kuhusu viwanja, alisema lingeshughulikiwa ila aliwashauri wanachuo kufanya mazoezi mengine huku wakisubiria suala hilo kupatiwa ufumbuzi. Suala la uzembe wa walinzi limepigiwa kelele kwani kumekuwepo na wizi wa mara kwa mara na upotevu wa mali za wanafunzi kama vile Laptop na pesa taslimu nalo amesema lingefanyiwa kazi mapema.

Aidha, Mwanachuo mmoja alisikitishwa na mavazi ya wanachuo kwa sasa ambayo yanaondoa hadhi ya vitivo wanavyovisomea vya Uongozi na Sheria hasa wakina dada ambao wamefikia hatua ya kuvaa ngou zinazowaacha wazi sehemu kubwa ya miili yao hasa vifuani na kupendekeza kuwa uwekwe utaratibu maalumu wa mavazi rasmi (Dressing code) hasa muda wa vipindi ili kuweza kuleta hadhi yao na kuwatofautisha na watu wa mitaani.


Saturday, November 24, 2012

KONGAMANO LA CHANGAMOTO ZINAZOKABILI MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU NA ATHARI ZAKE LAFANYIKA CHUO KIKUU MZUMBE

Kongamano hilo la aina yake lililojumuisha wageni kutoka vyuo vikuu mbalimbali (SUA, MOROGORO UNIVERSITY, RUCO na ST. JOSEPH) waliolikwa katika kongamano hilo kubwa kuwahi kutokea vyuoni liliendeshwa na Profesa Mchome (katibu Mkuu wa TCU) kwa kushilikiana na Ndugu Onesmas Laizer (Mwakilishi kutoka Bodi ya mikopo ya Elimu ya juu) kwa kuwasilisha mada mbalimbali zilizolenga kujadili changamoto zinazoikabili bodi ya mikopo katika utoaji na urejeshwaji wa mikopo na mstakabali wa changamoto hizo. 

Mada nyingi zimejadiliwa ila mada zilizoonekana kutawala mjadala huo ni pamoja na ucheleweshwaji wa mikopo hususani chuo Kikuu Mzumbe, utoaji wa mikopo kwa upendeleo hususani wanafunzi wanaosoma kozi za sayansi jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi kupata mikopo pasipo stahili, mfano baadhi ya wanafunzi wanaofaulu masomo ya sayansi ni wale waliosoma Shule nzuri kama Fedha, St. Marian nk. kuwa wanafunzi hawa wazazi wao wanakuwa na Uwezo wa kuwasomesha, Sera ya vipaumbele "Priorities" kwa baadhi ya kozi kujenga madaraja kwani wanaokimbilia mikopo ni watoto wa masikini ambao hulazimika kusoma kozi ambazo siyo chaguo lao na malipo ya "field studies kucheleweshwa na kutolipwa kwa viwango sahihi.

Akijibu hoja hizo Ndugu Laizer amesema kuwa suala la upendeleo si kweli ni fikra tu zilizojengeka miongoni mwa watu na wanafunzi kwani mikopo hiyo hutolewa kwa kuzingatia taarifa zilizojazwa na Mwanafunzi, kuhusu ucheleweshaji ameahidi kuwa maboresho yanaendelea ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa kunakuwa na mawasiliano ya karibu na vyuo ili kuwahisha matokeo ya wanafunzi mapema  na kuwa suala hilo litabaki kuwa historia tu. kwa upande mwingine amekiri na kumesema kuwa suala hilo inawezekana lipo japo si makosa ya bodi kwani wanaamini kuwa taarifa zinazowafikia bodi zinakuwa ni sahihi kwani zinapitia kwa watenadaji wa vijiji na mitaa wanowafahamu watu. Suala la malipo ya "field studies" hutegemea na asilimia ya mkopo anaoupata mtu, hivyo kutofautiana ni jambo la kawaida.

Aidha mapendekezo yametolewa juu ya uboreshaji, mapendekezo hayo ni pamoja na uongozi wa bodi kufanya ufuatiliaji wa karibu katika taarifa zinazojazwa na wanafunzi ili kuwabaini wadanganyifu pia kufuatilia wanafunzi wanaomaliza vyuo na kuhakikisha mikopo inarudi ili kuwawezesha wanafunzi walioko vyuo kutopata matatizo ya mikopo. Mapendekezo mengine yalikuwa ni kupunguza gharama za kutuma maombi ili kuwawezesha wazazi wa kipato cha chini kumudu gharama hizo na kubadilisha mfumo unaotumika wa sasa wa kutuma maombi kwa njia ya mtandao.

Akihitimisha Kongamano hilo Profesa Itika (Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo) amewashukulu Viongozi  (kutoka TCU, HESLB na NACTE) waliohudhuria kongamano hilo na Serikali ya wanafunzi kwa ujumla.

PICHA KATIKA MATUKIO 

Ndugu Onesmas Laizer akichokoza mada katika Kongamano la Changamoto  zinazowakabili  wanafunzi wa elimu ya juu na athari zake.

Mh. Hamis Mbawala (Waziri wa Wizara ya Mikopo) Serikali ya wanafunzi Mzumbe (MUSO) akitoa maonii.


Kutoka kushoto ni Rais wa Serikali ya wanafunnzi Chuo kikuu mzumbe (MUSO), Kaimu Mkuu wa Chuo kikuu Mzumbo, Profesa Mchome (Katibu Mkuu TCU) na Katibu Mkuu wa NACTE wakifurahia jambo wakati mwakilishi kutoka bodi ya Mikopo akiwasilisha mada.



 
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

IDADI YA WASOMAJI

RedEnvelope
. .

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...